NGUVU ILIYOPO KATIKA NENO LA MUNGU



NGUVU ILIYOPO KATIKA NENO LA MUNGU


   Karibu ndugu msomaji katika mfululizo wa masomo haya ya kibiblia kwa kutembelea www.injilikamiliyayesu.blogspot.com au facebook page “Injili Kamili YA YESU” ili kujifunza masomo mengi zaid ya Kimungu. Nakukaribisha katika somo hili jipya kwaajili ya kujifunza machache haya ambayo Mungu amenipa kibali kuyaachilia kwako kupitia kichwa cha somo kinachosema “NGUVU ILIYOPO KATIKA NENO LA MUNGU”.

 Tuanze na kutafakari maana Kamili ya neno kibiblia.

    Neno ni ujumbe wa Mungu ambao unaotumika na mwanadamu kwaajili ya kumfundisha na kumwongoza mwanadamu kuishi maisha matakatifu ya kumtafuta Mungu. Sambamba na kwamba neno la Mungu limehifadhiwa na mwanadamu kwa njia ya mandishi lakini kutokana na kukua kwa teknolojia hadi kwa njia ya sauti hili neno limehifadhiwa pia.

    Sasa basi neno hili ndilo ambalo Mungu ametupa kama sehemu ya msingi au njia ya mwanadamu kutatua matatizo yake kwa kulitumia hilo neno. Na hili neno pia baada ya mwanadamu wa mwanzo kuasi yaani Adamu na Hawa ndipo akamtuma mwanae wa pekee Yesu Kristo ili kuendelea kulitimiza neno lake kwa mwanadamu kwa njia ya agano jipya.

 Soma YOHANA 1:1-5Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika, ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza”. Maana yake pasipo neno katika maisha ya mwanadamu hakuna chochote kinachoweza kufanyika na hilo neno ndilo lililokuwapo toka mwanzo hata kabla ya mwanadamu kuwapo.

   Lakini sambamba na kuwa neno ni dira au mwongozo wa kumwongoza mwanadamu pia neno linauwezo wa kutumika kama silaha ya mwanadamu katika kuzipinga nguvu za ibilisi au shetani. Soma WAEFESO  6:11-13, 17Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuuweza kuzipinga hila za shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. 17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu”. Hapo tunaona katika mstari wa mwisho kuwa Neno ni upanga wa Roho maana yake mpiganaji yeyote anayepigana vita vya Rohoni akiwa na silaha hii ya neno la Mungu yupo katika nafasi kubwa ya kushinda vita yake kwa maana kila aendaye vitani lazima anakuwa ametwaa silaha ambayo itamsaidia katika kupambana kwenye vita hiyo.

    Pamoja na kuwa neno tunaweza kulitumia katika vita ya Roho lakini kuna kiasi cha neno hilo ambacho si kiwango cha idadi ndogo bali ni kuwa na neno kwa wingi. WAKOLOSAI 3:16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za Rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu”. Hivyo tunahitaji neno la Kristo liwe kwa wingi ndani yetu ili liweze kutufaa katika vita yetu ya Rohoni tunayopambana nayo.

   Swali: kwanini Neno la Mungu linatakiwa kukaa kwa wingi ndani yetu? 

Neno la Mungu linatakiwa kukaa kwa wingi ndani yetu kwasababu zifuatazo.
i.                    Neno la Mungu li hai.
ii.                  Neno la Mungu lina nguvu. Mwanzo 1:6

Kwanini neno la Mungu li hai?

a)      Kwasababu linafanya mabadiliko. ISAYA 55:10-11Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala haitarudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa  neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma”. Kwahiyo neno la Mungu linapo kuwa ndani ya mtu wa Mungu na mtu huyo akaliamini na kuliishi ndipo linapo mbadilisha na kuleta mfumo mwingine wa maisha ambayo ni ya Kimungu.

b)      Linatupa kushinda dhambi. ZABURI 119:11Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi”. Maana yake neno la Mungu linakuwa hai likinena ndani yetu kwaajili ya kutuzuia pale tutakapo kutenda dhambi neno lina tukemea na kutukumbusha kuwa jambo Fulani ni sahihi au sio sahihi mbele za Mungu.

c)      Linaweza kuleta majibu katika maisha yetu. LUKA 5:3-6Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akataka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni. Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki. Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu. Basi walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika”. Hapo tunaona jinsi neno lenye mamlaka ya jina la Yesu lilivyotoa majibu katika jambo lililoonekana kuwa mzingo kwa wanafunzi wake maana kwa usiku mzima walikesha bali pale tu walipo sikia na kutii neno la Kristo ndipo walipopata samaki wengi kiasi cha nyavu zao kuanza kuchanika. Ndivyo hata sisi leo neno la Mungu linavyoweza kufanya mabadiliko katika maisha yetu ambayo tunaona ya kwamba yamekufa au hakuna namna ya kutoka hapo kama vile Elimu, ndoa, kazi, n.k lakini neno la Mungu pekee linaweza kututoa katika mazingira hayo yote.

   Pamoja na kwamba neno la Mungu linauwezo wa kufanya mabadiliko hayo yote bado neno hilo linatakiwa liwe na uhai ndani yake yaani ule uhai uliopo katika neno ndio unaotupa kuishinda dhambi na kumshinda mwovu shetani. UFUNUO 12:11Nao wakamshinda kwa damu ya mwana-kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa”. Maana yake uhai wa neno unapatikana pale ambapo tunalitumia neno hilo kwaajili ya kuwashuhudia wengine pamoja na adui zetu na kuupata ule ushindi kwalo. 

    Swali: kwanini inafika wakati tunashindwa kulitumia neno la Mungu kama silaha katika mapito yetu? 

WAEBRANIA 4:2Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vilevile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwasababu halikuchanganyika na imani ndani yao waliolisikia”. Maana yake lazima neno liwe na imani ndani yake ili liweze kuleta mabadiliko kwahiyo isifike wakati ukamlalamikia Mungu kwa kusema mbona neno lake halijibu maombi yako lazima uangalie na imani yako iko wapi. Maana unaweza kutumia neno kumwomba Mungu juu ya hitaji lako lakini kumbe ndani yako bado unamwangalia shangazi, mjomba, baba, mama, mke, mume, n.k kuwa anaweza kukusaidia, hapo usitegemee kuona majibu katika maombi yako maana hao wote huwainua Mungu mwenyewe ili wakusaidie baada ya kuyaona maombi yako na sio kwa wewe kuwaona kama wana msaada kwako maana macho ya kibinadamu/ya nyama hutudanganya tu.

   NB: Pamoja na kwamba neno hili la Mungu tunalitumia kwaajili ya kushinda hila, mipango na vita zote ambazo shetani anainua ndani yetu lakini hata shetani analijua neno na anaweza kutumia neno hilo katika kutufanya sisi tuanguke Kiroho. LUKA 4:1-13………….. Akamwongoza mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake wakulinde; na ya kwamba, mikononi mwako watakuchukua, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe……….”. hayo yalikuwa ni maneno ya shetani akimjaribu Yesu baada ya kufunga kwa siku arobaini, swali ambalo unaweza kujiuliza ni wapi shetani alipata nguvu na mamlaka ya kutamka maneno mazito kama hayo jibu ni kwamba alipata katika neno hilohilo ambalo wewe unalijua. ZABURI 91:11-12Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe”. Hilo ndilo jambo ambalo linamfanya shetani aendelee kutawala maisha ya mwanadamu kila kuitwapo leo kwa sababu naye analijua neno.

       Kwa kumaliza niseme pamoja na kwamba sisi tunalijua neno na shetani analijua neno lakini bado sisi wanadamu tunayo mamlaka kubwa kuliko shetani katika kulitumia neno endapo tutaushika mstari kutoka KOLOSAI 3:16a maana kwa kule kuwa na neno kwa wingi ndani ya Yesu ilimfanya shetani aahirishe kazi ya kuendelea kumjaribu Yesu. Amen

Mungu awabariki.
By
Enea Msanga
eneamsanga@gmail.com
+255766966930/+255658443473
Karibu kwa maoni na maswali…………………………………

Comments

  1. Mafundisho haya ni ukombozi halisi nayo ni adimu Sana,
    Ni njia gani yawafikie watu wengi.!!!!!!!

    ReplyDelete
    Replies
    1. Mungu anatupenda sana na hakuna kitu cha kipekee na zawadi ya kipekee aliyotupa kama neno. 🙏🙏🙏🙏 Mungu atutie nguvu zaidi tudumu katika kulisoma neno daima

      Delete
  2. Tuzidi kumwomba Mungu ili kweli yake iwafikie wengi

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

KIJANA NA USAFI WA MAISHA YA KIKRISTO

WAJIBU WA KIONGOZI {P2}