TUMIA MAOMBI KAMA SILAHA.



TUMIA MAOMBI KAMA SILAHA:

       BWANA Yesu asifiwe!!!!!!!!

   Nawakaribisha katika somo hili la KUTUMIA MAOMBI KAMA SILAHA” kama ilivyonenwa katika

 WAEFESO 6:12Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama;bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya pepo wabaya katika ulimwengu wa Roho

   Maana yake vita tuliyonayo sisi Wakristo si katika mwili bali ni katika Roho maana yake kama vita vyetu vingekuwa ni vya mwili tungeandaa mapanga, visu, mashoka, bunduki, mishale na kila aina ya silaha za mwili. Lakini kwa sababu vita tulivyonavyo ni vya Roho ni lazima tutumie silaha za Rohoni ili kushinda vita hiyo maana silaha za mwili hazitatufaa kitu.

    Sasa kwa maana hiyo lazima tujue kuwa kama wapiganao vita vya mwili hutumia silaha tofauti tofauti na zenye uwezo tofauti kama SMG… hata sisi tulio na vita vya rohoni tunatakiwa kuwa na SMG… za Rohoni ili kuvipiga vita vilivyo vizuri.

  Ukisoma WAEFESO 6:11-13, 18.

  Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama”. 18 “kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;”

  Biblia katika kitabu hiki inatuonyesha kuwa tuvae silaha zote za MUNGU  maana yake Mungu ndiye mwenye Roho wa kutusaidia katika vita yetu na Biblia ipo wazi kwamba tukisha vaa silaha hizo ndipo tutaweza kuzipinga hila za shetani maana yake shetani hutujia kwa hila hivyo kama hatuna silaha za Rohoni hatutaweza kushinda hila hizo. Sasa ebu tuangalie silaha ya maombi kama Biblia inavyosema katika mstari wa 18.

    Maombi ni silaha ambayo inaweza kutusaidia katika kuzishinda hila za shetani lakini maombi hayo ni lazima tuombe kila wakati maana yake maombi tunayoomba kila wakati ndiyo ya kutusaidia katika kufanya ulinzi wa kupinga hila za shetani.

    MATHAYO 6:6

Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.

  MAOMBI ni mfumo wa kupeleka mahitaji yako mbele ya mtu ambaye unajua kuwa anaweza kuwa msaada kwako. Hivyo ili kupeleka maombi yetu kwa Mungu ni lazima yaambatane na sala. Sala huu ni mfumo wa kupeleka mahitaji yetu mbele za Mungu kwahiyo huwezi kupeleka  mahitaji yako mbele za Mungu bila sala. Sasa kwa wanadamu huwa wanahitaji barua ambayo ina kuwa na vipengele vyake. Na Mungu ameweka mfumo wa sala ambao una vipengele vyake ili kukamilisha maombi yako. Vipengele hivyo ni:-
           i.            Kuingia katika chumba cha ndani.
Katika kipengele hiki ni kuandaa mazingira ya kutengeneza utayari wa kwamba unaenda kuzungumza na Mungu ili kuondoa moyo wako na nafsi kuingiliwa na hisia nyingine zozote za kuvuruga mpangilio wako wa maombi.

         ii.            Kufunga mlango wako.
Maana yake ni kuziteka fahamu, hisia, akili na kumbukumbu zako ya kwamba unakwenda kuzungumza na Mungu. Hivyo kuwa katika mazingira pia ambayo yatakufanya uwe katika hali nzuri ya kuzungumza na Mungu maana yake hakuna hata hali au kelele zitakazo kufanya uache kuzungumza na Mungu.

         iii.            Kusali na baba yako aonaye sirini akujaze.
Hapa sasa ndio wakati ambao katika barua tungesema ni sehemu ya lengo la barua. Maana yake umesha yatengeneza mazingira ya utangulizi katika ulimwengu wa Roho  sasa unaanza kutiririka juu ya maombi na kupokea wakati huohuo katika ulimwengu wa Roho.

    Kwahiyo maombi yoyote ili yaweza kusikiwa na Mungu hutegemea sana mfumo au mtiririko au utaratibu au mpangilio au njia ulizotumia katika kuyawasilisha mbele za Mungu. Kama ambavyo katika barua ilivyotofauti barua ya kazi na barua ya kirafiki ndivyo ilivyo tofauti katika kuomba mbele za Mungu na kuomba kwa wanadamu wenzetu.


   Naomba kwa leo niishie hapa tutaendelea muda mwingine. Nakaribisha maoni. ila kwa masomo zaidi tembelea www.injilikamiliyayesu.blogspot.com au facebook page “Injili Kamili YA YESU”

 

Comments

Popular posts from this blog

NGUVU ILIYOPO KATIKA NENO LA MUNGU

KIJANA NA USAFI WA MAISHA YA KIKRISTO

WAJIBU WA KIONGOZI {P2}